Tangu sasa tutasimama wima na kutembea kwa miguu yetu badala ya kupinduka na kuwa miguu juu vichwa chini. Viwanda vitakuja, na fedha zitakuja, lakini msingi wake ni WANANCHI na JUHUDI yao na hasa katika KILIMO. Hii ndiyo maana ya kujitegemea. Kwa hiyo basi, mkazo wetu na uwe:-
(a) Ardhi: Kwa kuwa uchumi wa Tanzania unategemea na utaendelea kutegemea kilimo na mifugo, Watanzania wanaweza kuyaendesha maisha yao barabara bila ya kutegemea misaada kutoka nje kwa matumizi bora ya ardhi hiyo. Ardhi ni ufunguo wa maisha ya binadamu kwa hiyo Watanzania wote waitumie ardhi kama ni raslimali yao kwa maendeleo ya baadaye. Kwa kuwa Ardhi ni mali ya Taifa, Serikali ni lazima iangalie kuwa ardhi inatumiwa kwa faida ya Taifa zima na wala isitumiwe kwa faida ya mtu binafsi au kwa watu wachache tu.
(b) Watu: Kuiwezesha siasa ya kujitegemea itekelezwe vizuri,wananchi ni budi wajengwe moyo na shauku ya kujitegemea.Wajitegemee katika kuwa na chakula cha kutosha, mavazi yakufaa na mahali pazuri pa malazi.Katika nchi yetu kaziiwe ni kitu cha kujivunia. Bali uvivu, ulevi na uzururajiuwe ni jambo la aibu kwa kila mwananchi. Katika upande wa ulinzi wa Taifa, wananchi wawe macho na vibaraka waliomo nchini ambao wanaweza kutumiwa na maadui wa nje wenye nia mbaya ya kuliangamiza Taifa hili na wawe tayari kulilinda Taifa inapolazimika kufanya hivyo.
(c) Siasa Safi: Msingi wa siasa ya kujitegemea lazima uambatane na siasa ya Ujamaa ya TANU. Ili kuzuia unyonyaji ni lazima kilamtu afanye kazi na aishi kwa jasho lake yeye mwenyewe. Na ili kuleta usawa wa kugawana mapato ya nchi ni lazima kila mtu atimize wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii zake zote. Asiweko mtu wa kwenda kwa ndugu yake na kukaa kwa muda mrefu bila kufanya kazi kwa sababu atakuwa anamnyonya yule ndugu yake.

